Pages

Thursday, November 13, 2014

Je Unafahamu NDOA yako inahitaji NiNi??

Katika siku za hivi karibuni, suala la kuvunjika kwa ndoa za watu mbalimbali limekuwa kama utamaduni ambao tunatakiwa kuzidi kuuzoea haraka kwakuwa limeendelea kuchukua kasi ya ajabu. Kuanzia ndoa za watu maarufu hadi wasio maarufu, watu walio na uwezo na hata wasio na uwezo pia, hakuna mahali ambako kumekuwa salama linapokuja suala la wawili walioungana kuishi katika kiapo chao wanachokitoa siku ya kufunga ndoa cha "ndio nimekubali"
Ukosefu wa uvumilivu baina ya wanaooana, kuolewa pasi na kujiandaa kisaikolojia, kuolewa au kuoa kwa malengo fulani fulani na mambo mengine kama hayo, zimekuwa miongoni mwa sababu ambazo zimekuwa zikipelekea kuvunjika kwa ndoa nyingi, tena zingine zikiwa zingali changa sana. Lakini je, unajua kuwa kuna uwezekano mkubwa wa watu wawili kuishi miaka mingi zaidi katika ndoa, kiasi cha kuweza kutimiza ile ahadi ya :ndio nimekubali kuwa naye hadi kifo kitakapotutenganisha?
Hapa, ni mambo kumi ambayo ukiyazingatia, yanaweza kabisa kukufanya uishi katika kiapo chako unachokitoa siku ya kufunga ndoa

1. Fahamu, kubali na amini kuwa ndoa ni raha na karaha:
Ndio, hatua ya kwanza kabisa ya kujiandaa kuhakikisha kuwa unaishi katika kiapo chako cha "ndio nimekubali", ni kutambua kuwa, maisha ya ndoa ni maisha yaliyojaa raha na karaha. Ikumbukwe kuwa, ndoa, ni muunganiko wa watu wawili ambao kila mmoja alizaliwa, kukulia na kuishi katika familia, utamaduni na aina ya maisha tofauti na ya mwenzake. Katika muktadha kama huu, aghalabu, ni vigumu kutegemea kuwa, wawili hawa watakuwa sawa sawa kimitizamo, fikra na hata utendaji wa mambo mbalimbali kuhusiana na ndoa yao. 
Ikumbukwe pia kuwa, kuna msemo usemao "kama watu wawili watakuwa wakikubaliana katika kila jambo, ni dhahiri kuna mmoja kati yao asiyefikiri" … na kwakuwa maisha ya ndoa ni lazima kila mmoja afikirie, basi ni lazima mikwaruzano ya hapa na pale iwepo. Hata hivyo, ni vyema pia kutambua kuwa, kuna mambo mengi ambayo yanawaunganisha, yaliyo mema na yenye kufurahisha, ambayo mnatakiwa kuishi kwayo, huku mkiamini kuwa, karaha za hapa na pale, zinatakiwa kuwemo ili mzidi kuwa imara kiimani na hata kihisia.
2. Tumia nguvu ya mguso wa mikono yako:
Ndio, mara ya mwisho wewe kumshika mke/mume wako mkono ilikuwa lini? Iwe kwa kusalimiana au kwa namna yoyote ile?
Kushikana mikono, ni moja ya mambo ambayo wengi huyafanya wanapokuwa wapenzi. Ni aina na ishara ya kuonyesha ukaribu wa aina fulani baina ya watu wawili. Ikiwa ulikuwa unamshika mpenzi wako mkono enzi zenu za uchumba na upenzi wa kawaida na ukawa unajisikia ukaribu naye kwa kufanya hivyo, iweje leo hii unapokuwa naye ndani usitishe zoezi hili? 
Kuushika na kuuchezea chezea mkono wa mwenza wako, na hususan sehemu ya viganjani, ni jambo dogo, lakini ambalo linaweza kurejesha kumbukumbu za nyuma wakati mlipokuwa mkifurahia mahusiano yenu kama wapenzi. Ni jambo ambalo linaweza kukukumbusha mambo mengi ambayo mliahidiana mazuri, mambo mengi mazuri ambayo mlibaini yanatakiwa kuwaunganisha kabla hamjaungana, na kwa hakika si jambo la kupuuzia japo laweza onekana lisilo na maana.

3. Kujihisi kutokubalika:
Ni lini mara ya mwisho umemwambia mpenzi wako "Asante" … na ukamuangalia anapokeaje neno hilo? Au wewe unajisikiaje mwenza wako anapokwambia asante? Kukubali na kukubalika, ni miongoni mwa mambo ambayo huwafanya wapenzi kujihisi kuwa karibu zaidi kwa kuona wanatambulika na kuthaminiwa. Upo ushahidi wa wazi kuwa kuna watu walithubutu kujiondoa mahali walipo kwakuwa walihisi hawakubaliki kwa namna yoyote ile, na kwa hakika, ni hali yenye kuudhi na kuvunja moyo pia.
Haijalishi ukubwa au ubora wa kitu, kwa wawili kupeana asante iwe kwa chakula, zawadi au kitu chochote kile, utamaduni wa kushukuru, humfanya mwenza wako kujiona mwenye kukubalika na hilo humpa nguvu ya ziada ya kuthamini kumkubali kwako.
4. Tenganisha maisha ya nyumbani na nje ya nyumba:
Hebu kaa na ujikumbushe mara ya mwisho ilipokutokea kwamba ile unafika tu nyumbani, swali la kwanza lilikuwa "fulani ni nani" au kwanini hiki au kile nk?
Ikweli ni kwamba, nyumbani kwako ni sehemu ambayo unatakiwa kupata kila unachokihitaji ili kupumzisha kichwa chako. Nyakati kama hizi ambazo maisha yamekuwa yakienda kasi sana huku uhangaikaji ukiwa ni wenye kukwaza wengi wawapo makazini, kitu pekee ambacho mtu unaweza kukihitaji pindi utokapo huko, ni kupokelewa kwa kupewa pole yenye kumaanishwa na mtoaji. Na ikiwa hivi ndivyo inavyotokea, hakika nyumbani panakuwa mahali pekee ambako mwenza wako anapa-miss sana awapo nje, na atapo penda kukimbilia kila apatapo upenyo.
5. Amsha hisia za ukaribu:
Unakumbuka enzi zile za upenzi wenu? Ambako kila mlipokaa mlitamani muwe mmeegemezeana mabega yenu? Au mlipokuwa mkahawani kila mtu upande wake, lakini miguu ikawa imegusana chini ya meza ya chakula? Unakumbuka hisia ulizokuwa unazipata kwa nyakati kama hizo? Zirejeshe haraka nyakati hizi. Haitoshi tu kukaa karibu na mwenza wako, bali hakuna ubaya mkigusishana mabega mnapokuwa karibu, au hata kutekenyana kwa vidole vya miguu yenu mnapokuwa mmekaa pande tofauti za meza. Inasaidia kurejesha hisia zenu za wakati mlipokuwa kwenye wakati ulio bora kabisa wa urafiki wenu.

6. Acha u-mimi
Mimi najua, mimi naweza, nilishasema …. na maneno kama hayo au mambo kama hayo, si mambo sahihi katika maisha ya ndoa. Ndoa ambayo tumeshasema ni muunganiko wa watu wawili, inajumuisha watu wenye akili zenye kufanya kazi karibu sawa sawa, na ndio maana mioyo yao ikakubali kuungana. Kujiona unajua kila kitu, hakuwezi kamwe kukusaidia kuishi katika kiapo cha "ndio nimekubali"
7. Nguvu ya Ninakupenda:
Siku hizi maisha yamekuwa kuhangaika pande zote mbili, kwahiyo mara nyingi, watu tunakurupuka kwa pamoja kwenda mihangaikoni. Ila ikiwa nafasi inapatikana, hakikisha unaweka ujumbe wa "Nakupenda" kwa mwenzako kila mahali ambako unaamini itakuwa rahisi kwa yeye kuona. Kwenye kioo cha kuvalia chumbani, kwenye bahasha ya zawadi, au kumtamkia wakati unamuacha au anakuacha kazini kwako.
8. Tafuta ukijani ulionawiri:
Ndio, si imeshaainishwa hapo awali kuwa maisha ya ndoa ni raha na karaha? Iwe karaha zitokanazo na mwenzako au zitokanazo na shinikizo la maisha ya nje ya nyumbani, pale unapohisi unahitaji kupata ukijani mpya ndani ya moyo wako, jipe nafasi ya namna hiyo. Kafanye mazoezi, nenda katembelee mbuga, au ndugu na jamaa kwa muda kadhaa. Hii itakufanya upate wasaa mzuri wa kuchambua na kuyarejesha yale yaliyowaunganisha kuliko karaha ndogo ndogo za maisha. Na pale mwenza wako anapohitaji kufanya hivyo, ni vyema kuelewa na kumruhusu pia.

9. Busu:
Kumbuka ulivyokuwa ukimbusu zamani na akapata hisia za busu hilo. Rejea kufanya hivyo kila wakati na ukimaanisha hivyo kweli, kwani itaendelea kumfanya akumbuke nyakati zenu za awali mlipokuwa mnaona furaha tu mbele yenu.
10. Kuwa mbunifu:
Mtumie ujumbe wa maneno kwa njia ya simu ukimueleza mambo unayoona yatamfanya atabasamu na kuifanya siku yake kuwa nzuri. Kwa mtindo huu hakika atakuwa akitamani akuone siku nzima.

No comments:

Post a Comment