UNAJUA NAFASI YA WATOTO KATIKA NDOA ??


Kawaida watu wanapozungumzia kuhusu suala la ndoa, kipengele cha watoto huchukua nafasi kubwa na ya muhimu katika mazungumzo ya ndoa na ujengaji wa misingi bora ya familia. 
Kwanza kabisa unakumbuka kuwa kupata watoto ni moja ya lengo la ufungaji maagano ya ndoa. Mwenyezi Mungu amependa kumkabidhi mwanadamu jukumu hilo la kukiendeleza kizazi cha wanadamu. Ni kutokana na upendo mkuu alionao Mungu, kamuumba mwanadamu ili kumshirikisha upendo huo. Unapopewa jukumu la kuendeleza kizazi cha mwanadamu, nakualika ukumbuke kuwa hilo linatendeka katika tendo la kiupendo mkubwa.
Mwenyezi Mungu kaumba ulimwengu na kapanga utaratibu wa kufuata. Unapokwenda nje ya utaratibu huo unakuwa unavuruga mpango wa kimungu, hivyo unakuwa unatenda dhambi. Watoto wanapatikana kihalali katika tendo la ndoa. Nikisema tendo la ndoa simaanishi mahusiano tu, bali namaanisha tendo lilohalalishwa kisheria za dini/mahakama, ndio sababu linaitwa tendo la ndoa.

Tendo hilo linafanyika kwa upendo hasa sababu pia chanzo chake ni upendo. Kwa hivi mtoto unakuwa ni tokeo, au tunda la upendo kati ya baba na mama. Inapotokea unaendeleza kizazi nje ya ndoa, bado mtoto huyo anakuwa ni tunda la upendo, isipokuwa tendo lenyewe linakuwa halijahalalishwa.  
 Watoto wanakamirisha ule mkusanyiko wa sehemu tatu muhimu ndani ya familia: yaani baba, mama na watoto. Watoto wanaongeza furaha ya familia, wanachangamsha familia. Lakini zaidi hasa watoto wanasaidia wazazi kukomaa kiutu, kiimani na kijamii. Unapoitwa baba au mama, unafahamu wajibu unaobeba wa kulea vema watoto, kuwatafutia mahitaji yao ya msingi na kuishi kwa heshima kadiri ya hadhi ulioyonayo. Kuwa makini zaidi katika kuwatafutia wanao furaha na maisha bora ya baadae.
Kuna vitu ulivyozoea kufanya awali lakini sasa huwezi kuvifanya tena. Hii ni neema Mwenyezi Mungu anakupatia katika kukua kwako siku hadi siku, kuongeza ukarimu, upendo, huruma, na kuifanya dunia kuwa paradiso ndogo kwa ajili ya watoto na kizazi kijacho.

Ikitokea watoto hawapatikani katika ndoa, msikate tamaa, endeleeni kutafuta kwa njia za haki na halali. Na tambueni ya kuwa, ndoa na familia bado inakuwa na hadhi yake na ukamilifu wake wa kuitwa ndoa na familia sababu hata kama watoto hamjapata, moyoni na kwa upendo mkuu mnao watoto kwa tamaa mliyonayo na kwa nia njema.


0 comments:

Copyright © 2013 Owned and Managed by Bouner Disneysorata Tanzanite! All right Reserved..