JE UNAJUA NAMNA YA KUEPUKA MAUMIVU KATIKA NDOA/MAPENZI ?




Zifuatazo ni mbinu ambazo zitakusaidia kuyabadilisha maumivu yako ya kimapenzi kuwa furaha.
JIFUNZE KUSAMEHE NA KUSAHAU
Hakuna jambo ambalo hutuliza fikra na hisia za mapenzi kama kukubali kumsamehe yule aliyekuudhi kabla hata hajakuomba msamaha na kuamua kusahau yote yaliyotokea. Yawezekana wengi mtasema haiwezekani. Inawezekana na wote waliojaribu mbinu hii walifanikiwa.
Marafiki, lazima kila mmoja aelewe kwamba unapokasirika au kuumizwa, anayeteseka siyo yule aliyekusababishia maumivu bali ni wewe mwenyewe. Hasira au maumivu ya kimapenzi huwa kama moto mkali ambao huitafuna taratibu nafsi ya mhusika.
Ukisamehe maana yake unaupa moyo na akili yako nafasi ya kupata sehemu ya kutulia na kuuzima moto ambao tayari ulishaanza kukolea ndani yako. 



                                                   BADILISHA MAZINGIRA/ MARAFIKI
Baada ya kuumizwa na mwandani wako, mbinu ya kubadilisha mazingira na marafiki husaidia sana kukupa nguvu ya kukabiliana na msongo unaoweza kukusababishia madhara makubwa.
Unaweza kubadilisha mazingira kwa kusafiri, kubadilisha mpangilio wa chumba chako cha kulala na kuondoa vitu vyote vinavyoweza kukukumbusha hisia chungu za maumivu. Taratibu utaona akili yako ikianza kusahau maumivu.
Yawezekana pia kuwa mpenzi wako ulishamtambulisha kwa marafiki zako nao wakamuona kama sehemu ya familia. Ukiendelea kujumuika na marafiki hao, watakuwa wanakukumbusha hisia chungu zitakazoendelea kukutesa, jiweke karibu na marafiki wapya wasiojua historia yako ya mapenzi, watakuwa sehemu ya faraja kwako.


                                                                JIPENDE, JITHAMINI
Utafiti wa kisaikolojia umebaini kuwa baada ya kutendwa kimapenzi, watu wengi hujishusha thamani na kudhani huenda wana upungufu, kasoro au udhaifu fulani ndiyo maana wapenzi wao wakawasaliti na kutoka kimapenzi na watu wengine.
Kama ni mwanamke, muda wote atashinda kwenye kioo akijikagua kama ana kasoro kwenye sura na mwonekano wake. Mwanaume vivyo hivyo, atashinda akijiuliza kuhusu uwezo wake wa kumfurahisha mwenza wake faragha au uwezo wake wa kifedha.
Kuyabadili maumivu haya kuwa furaha, jitazame kwa jicho la tatu na kujiambia kuwa wewe ni mzuri, una umbo zuri, unajua kukidhi haja za mwenzako mkiwa faragha na kwamba hauna kasoro yoyote. Jipe nafasi ya kushughulikia maisha yako ya baadaye na suala la mapenzi achana nalo kwa muda mpaka utakapokuwa umetulia.
Kujipenda na kujithamini kuende sambamba na kuboresha mwonekano wako, hakikisha muda wote unakuwa msafi na mazingira unayoishi pia yanakuwa masafi.


                                                      SITISHA MAWASILIANO
Unapokuwa na maumivu ndani ya moyo wako, jambo la busara ni kukaa mbali na kusitisha mawasiliano ya aina yoyote na yule aliyekusababishia maumivu hayo. Wengi hufikia hatua ya kubadili namba zao za simu ili kupata muda wa kutafakari mustakabali wa uhusiano wao.
Kama alikuwa rafiki yako kwenye Facebook au Twitter, ‘block’ mawasiliano naye, kama ni kwenye simu sitisha kumtumia ujumbe mfupi au kumpigiapigia simu, iache akili yako ndiyo iamue kama bado unahitaji kuendelea kuwa naye au la.
Hata kama njia uliyokuwa unapita kwenda kwenye shughuli zako za kila siku ilikuwa inakufanya ukutane naye, badilisha njia na ratiba yako kwa jumla.


                                                  USITAFUTE WA KUZIBA PENGO
Kosa ambalo wengi hulifanya baada ya kutendwa na wapenzi wao, ni kukurupuka na kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na watu wengine muda mfupi baada ya kuumizwa. Badala ya kupunguza maumivu, utajikuta ukiongeza ‘stress’ kichwani kwani huyo unayedhani atafaa kuziba pengo, anaweza kuwa na maovu kushinda hata huyo aliyekuumiza.
Jipe nafasi ya kukaa mwenyewe na kufikiria maisha yako ya baadaye, amini kwamba maisha yanawezekana hata ukiwa peke yako, kubaliana na kilichotokea na jiambie kuwa hutaki kurudia makosa kwa kuanzisha uhusiano na mtu atakayeuchezea moyo wako.


                                                      JIPE ZAWADI 
Huenda wengi wakashangaa kwamba inawezekanaje kujipa zawadi mwenyewe? Inawezekana. Tembelea duka linalouza zawadi za kimapenzi kama maua, kadi nzuri, midoli au chocolate na jichagulie unayoipenda zaidi. Jiambie kuwa hakuna anayekupenda zaidi ya jinsi unavyojipenda mwenyewe, jipongeze kwani maumivu hayatajirudia tena. 
Ukizingatia dondoo hizi, utaona jinsi maumivu yanavyoisha ndani ya moyo wako na kuipa nafasi furaha kuchanua kama maua mazuri ya waridi yachanuavyo.




0 comments:

Copyright © 2013 Owned and Managed by Bouner Disneysorata Tanzanite! All right Reserved..